'''Muhtasari wa Kwanza wa Ukusanyaji wa Maoni Kuhusu Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Maadili'''
Utangulizi kuhusu Jumuiya
Jumuiya ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili ni kundi kubwa la watu wanaongea au kutumia lugha ya Kiswahili. Watu hawa mara nyingi wanatokea katika ukanda wa maziwa makuu na sehemu nyingine za mashariki na kusini-mashariki mwa Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, baadhi ya sehemu za Malawi, Somalia, Zambia, Msumbiji and the Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo (DRC). Kiujumla lugha ya Kiswahili imekuwa ni lugha inayojulikana na ni lugha rasmi ya kiofisi kwa baadhi ya nchi za Kiafrika kama vile Tanzania, Kenya, Uganda, and DRC Congo. Umaarufu wa lugha ya Kiswahili umekuwa kuongezeka tangu pale jumuiya ya SADC iliporasimisha Kiswahili kuwa lugha yake ya kiofisi ya nne mnamo mwaka 2019. Shirika la Wikimedia Foundation lina tolea la kiswahili la Wikipedia iitwayo Wikipedia Ya Kiswahili na kadiri ya takwimu za tar 11 Mei 2020 saa 17:22 jioni Wikipedia ya Kiswahili ilikuwa na wastani wa wahariri hai 137, wakabidhi 11, makala 58,868 , na ukubwa wa baiti 120,241. Baadhi ya makundi rasmi (Makundi ya Wanawikipedia yanayotambuliwa rasmi na shirika la Wikimedia Foundation) yenye kazi ya kuhariri, kuunda maudhui, kuchangia na kutunza Wikipedia Ya Kiswahili ni pamoja na Wikimedia Community User Group Tanzania, Jenga Wikipedia ya Kiswahili na Wikimedia community User Group Uganda ambapo makundi haya yanaundwa na watu wa aina mbalimbali kama vile Wanawake, Wanaume, Wanavyuo, Madaktari, Wachungaji, Wanaastronomia, walimu, wakufunzi, wapendateknolojia na watu wengine mabalimbali wapendao elimu huria.
Muhtasari wa Sera za Mienendo ya tabia katika Jumuiya
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa katika Wikipedia ya Kiswahili, inaonekana kuna Mwongozo ambao unatumika kuratibu shughuli mbalimbali za mtandaoni za Wikipedia ya Kiswahili kama vile namna ya kuchangia katika Wikipedia hiyo, umaarufu wa mada zinazotakiwa kuandikwa ndani yake na namna mtu anavyotakiwa kujiheshimu pindi anapochangia katika Wikipedia hiyo. Changamoto mojawapo inayojitokeza ni kwamba sera au mwongozo huo haujulikani sana na wachangiaji wa Wikipedia ya Kiswahili bali unajulikana na wachangiaji hai wachache wakiwamo wakabidhi. Utafiti unaonesha kuwa mwongozo huo ulitengenezwa na baadhi ya watumiaji wa Wikipedia Ya Kiswahili hapo awali pia baadhi yao ni watumiaji wa Kiswahili kwa kujifunza na si waswahili wazawa. Ingawa inadaiwa kuwa mwongozo huo ulitengenezwa na baadhi ya watumiaji wa Kiswahili wenyewe, baadhi ya maudhuo yake yanaonekana kufanana, kutoholewa au kutafsiriwa kutoka Wikipedia ya Kiingereza. Hii ni kutokana na uchache wa wachangiaji hai wa Wikipedia ya Kiswahili na idadi ndogo ya wakabodhi ambapo kuna wastani wa wakabidhi 4 kati ya wakabidhi wote 11 wanaoweza kufuatilia mwenendo wa uchangiaji katika Wikipedia ya Kiswahili na wanaoweza kusaidia kutengeneza na kufuatilia sera za mambo ya miongozo.
Mchakato wa Uwezeshaji
Wengi wa Wanawikipedia ya Kiswahili wapo katika mitandao ya kijamii na hufuatilia kurasa za kijamii za jumuiya kama vile katika WhatsApp na katika kurasa za facebook. Katika mchakato wa kukusanya maoni ya wanawikipedia kuhusu Mwongozo wa kimataifa wa Mwenendo na Maadili, kiungo chenye taarifa za ujumla kuhusu mradi huo zilitumwa katika kundi sogozi (kundi la WhatsApp) ambako mjadala ulianzishwa kuruhusu wadau kutoa maoni juu ya kile walichokuwancho kichwani kuhusu kuanzishwa kwa mwongozo huo. Kutokana na kwamba sio Wanawikipedia ya Kiswahili wote walikuwa katika kundi la WhatsApp,baadhi ya wadau walipendekeza kwamba mjadala uhamie katika ukurasa wa majadiliano wa Wikipedia ya Kiswahili ambako watu wengi wangepata fursa ya kutoa maoni yao. Kwa kufuata ushauri huo, basi mjadala ulihamishiwa katika ukurasa wa majadiliano wa Wikip[edia Ya Kiswahili, matokeo ya hatua hiyo hayakuwa ya kuridhisha kwakuwa si watu wengi walijitokeza kuchangia mawazo yao katika ukurasa wa majadiliao wa Kiswahili na pia njia hii ilionekana kuongeza ugumu kidogo kwa watu kuuliza na kupatat ufafanuzi wa papo kwa papo kabla hawajaingia hatua ya kutoa maoni yao. Baada ya juhudi hiyo kutozaa matunda kwa jinsi ilivyoatakiwa, njia nyingine ya kupata maoni ya wadau ilianzishwa, nayo ilikuwa ni fomu ya dodoso ya google ambayo ilikuwa na baadhi ya maswali machache ya kuongoza katika utoaji wa maoni, lakini bado mwitikio wa watu haukuwa mkubwa kwa kuwa watu wachache walishiriki kama ambavyo itaelezwa hapo chini katika kipengele cha takwimu.
Changamoto hizo zilisababisha kubadili namna ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau ambapo sasa njia iliyotumika ni mawasiliano ya mtu mmoja mmoja kwa njia ya simu na kwa njia hii watu waliweza kueleweshwa zaidi na hivyo walitoa mawazo yao kuhusu Mwongozo wa Kimataifa wa Mwmenendo na Maadili. Njia hii ya ukusanyaji wa maoni kwa mtu mmoja mmoja kwa njia ya simu na kwa nia ya ana kwa ana ilionekana kufaa na ilitatua baadhi ya changamoto ambazo baadhi ya wadau zilikuwa zikiwakumba kama vile ukosefu wa intaneti ambayo ingesaidia watu kushiriki katika mijadala ya mitandaoni kama vile katika WhatsApp na katika ukurasa wa majadiliano wa Wikipedia Ya Kiswahili.Ilikuwa ni nafasi mjema ya kutuunganisha na kujadiliana kama wadau wa Wikipedia ya Kiswahili na wengi walionekana kufurahishwa na njia hiyo.
Pamoja na kwamba njia hiyo ilizaa matunda, ilikuja na changamoto moja kwamba haikuwa rahisi kuwa na namba za wachangiaji wote wa Wikipedia ya Kiswahili na hivyo ilibidi njia nyingine zaidi itumike kuongeza wigo wa watu kutoa maoni yao. Njia hiyo iliyoongezwa ilihusisha utumaji wa ujumbe kwa wachangiaji hai wa Wikipedia ya Kiswahili wapatao 106 wa kuwaalika kutoa maoni yao kuhusu utengenezaji wa mwongozo huo. Juhudi hiyo nayo haikuzaa matunda kwa muda mwafaka maana hadi muda wa ukusanyaji wa maoni ulipoisha hakukuwa bado na maoni mengi ya wadau. Mwisho ukusanyaji wa maoni ulielekezwa kwa wadau weengine wa Wikipedia ya Kiswahili ambao walikuwa wanawikipedia kutoka Uganda, Kenya, Burundi na Kenya kwa kutumia fomu ya dodoso ya Google ambapo maoni yao yalikusanywa na kurekodiwa.
Maoni ya Wanajumuiya
Kiujumla zoezi la kukusanya maoni ya Wanawikipedia ya Kiswahili lilienda vizuri na idadi nzuri ya watu walijitokeza kutoa maoni yao kuhusu Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Maadili wengi wao wakisema ni jambo zuri kuwa na kitu kinachojaribu kuwaunganisha Wanawikipedia katika mambo ya msingi ili mradi kama mwongozo huo utazingatia na kuheshimu utamaduni wa jumuiya husika vilevile kuheshimu sheria na kanuni za nchi husika. Zaidi ya yote walisema mwongozo huo utaweza kusaidia wanawikimedia kujisikia huru kuchangia katika miradi ya Wikimedia Foundation huku wakiwa na uelewa wa kutosha juu ya nini kinachukuliwa kuwa ni sawa kufanya na kipi hakichukuliwa kuwa sawa wakati wa uchangiaji katika miradi mbalimbali ya Wikimedia.
Kwa upande mwingine baadhi ya washiriki katika utoaji wa maoni walisema hawaoni umuhimu wa kuwa na mwongozo huo kwakuwa ni kama miongozo yote miwilo ule wa Kiswahili na mwongozo mpya wa kimataifa unaokusudiwa vitafanya kazi karibia moja, na kwamba inaweza kusababisha mkanganyiko wa kuhusu mwongozo upi wa kuufuata hasa pale inapotokea kuna mkanganyiko fulani.
Katika mchakato mzima wa ukusanyaji wa maoni, watu tofauti walitoa mawazo yao mbalimbali kama ifuatavyo.
Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo (UCoC) na Maadili inatakiwa kiwe ni chombo kinachojieleza. Kutokana na uelewa mdogo wa mambo yahusuyo unyanyasaji, ilipendekezwa kuwa UCoC ujaribu kuwaelimisha watu kwa kutoa maana dhahiri juu ya ‘‘unynyasaji’’ unamaanisha nini hasa katika muktadha wa miradi ya Wikimedia Foundation. Kwa mujibu wa baadhi ya washiriki, itasaidia kuongeza uelewa kuhusu mada zihusuzo unyanyasaji kwa kuwa kwa sasa inaaminika bado kuna uelewa mdogo kuhusu mada hizo miongoni mwa Wanawikipedia na pia uelewa mdogo wa kujua kipi mtu mmoja akimfanyia mwingine chaweza kuchukuliwa kama ni unyanyasaji. Sambamba na hilo, baadhi ya wadau walipendekeza kuwe na Maswali yanayoulizwa mara kwa mara kuhusu UCoC pamoja na majibu yake ili kutoa majibu ya haraka kwa maswali ya mara kwa mara yaulizwayo na wanajumuiya.
Kiujumla idadi kubwa ya washiriki walipendekeza kuwe na namna ambayo UCoC ijali heshima, ulinganifu na utunzaji wa utofauti wa kitamaduni, kijamii, kidini na pia mwongozo huo uendane na taratibu pamoja na sheria za nchi husika. Kwa nyongeza zaidi ilipendekezwa kuwa UCoC usiwe na sera na utekelezaji unaojaribu kufanya vitu fulani vya kitamaduni kuwa ni kitu kimoja kwa watu wote , kwa mujibu wa washiriki hii itasaidia kueousha migogoro ya kisheria na uvunjifu wa desturi kwa mamlaka husika. Katika suala la faragha, baadhi ya watu walipendekeza kuwa kwa masuala yahusuyo unyanyasaji kusiwe na namna ya kuweka taarifa binafsi za wachangiaji wa miradi ya Wikimedia hadharani, badala yake nafasi ya watu kuonywa na kubadilika itolewe ili watu wenye mapenzi mema wapate kujirekebisha wenyewe.
Baadhi ya watu pia walitoa maoni yao kuwa nyenzo za kujifunzia masuala ya uchangiaji katika Wikipedia na miradi mingine ya Wikimedia hazijulikani na wachangiaji walio wengi bali na wachache kama wachangiaji wazoefu. Hivyo pendekezo lilitolewa kuwa mwongozo wa UCoC uwe na nyenzo muhimu kama vile miongozo au nyezo za kujifunzia mtandaoni na nyenzo nyingine zinazohitajika katika kujenga maarifa zaidi kwa wanawikimedia ili kusaidia kuepusha watu kuvunja sheria mbalimbali bila ufahamu timamu.
Ili kuhakikisha kuwa mwongozo wa UCoC utakuwa wenye kueleweka na kila mmoja, wengine walipendekeza kuwa kuwa na maelekezo rahisi katika mfumo wa ‘‘FANYA’’ na ‘‘USIFANYE’’ pamoja na maelezo ya kwanini inashauriwa kitu fulani kuchukuliwa ni chenye kukubalika au la. Pia jambo lingine lililopendekezwa ni kwamba itakuwa vema kam kutakuwa na toleo la Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Maadili kwa Lugha ya Kiswahili kwaajili ya kurahisisha uelewa.
Ilipendekezwa pia kuwa watu wasizuiliwe kukosoa vitu vyenye msingi ili kuwa na maudhui bora katika miradi ya Wikimedia Foundation hasa kwa zile mada zinazoonekana kuwa na mkanganyiko fulani. Ukosoaji ni vema ukaangaliwa kwa umakini mkubwa ili kubaini iwapo ulifanyika kwa lengo jema la kuboresha maudhui.
Ingawa bado haijawa dhahiri jinsi mwongozo wa UCoC utakavokuwa katika uhalisia wake, baadhi ya watu walipendekeza kuwa mwongozo huo utumie lugha rahisi na yenye kueleweka kwa watu wote kuanzia kwa watu ngazi ya chini mpaka watu wa ngazi ya juu na mwongozo huo ujitahidi kukubalika katika jumuiya mahalia huku ukijitahidi kufikia vigezo vya kimataifa. Sambamba na hilo, utekelezaji wa mwongozo huo unatakiwa kuwa sawa kwa jumuiya zote na pasiwe na ubaguzi wa kitaifa, kijinsia, kielimu na aina yoyote ya kibaguzi.
Mbali na mawazo ya wadau yaliyoelezwa hapo juu, yafuatayo ni maoendekezo mbalimbali yaliyotolewa na watu mbalimbali wakati wa mchakato wa ukusanyaji wa maoni.
Mwongozo wa kimataifa wa Mwenendo na Maadili inabidi upatikane katika lugha za jumuiya husika ili kurahisisha uelewa wa maudhui yake. Pia ili kuhakikisha kunakuwa na namna rahisi ya kutoa taarifa za matukio ya unyanyasaji, wadau walipendekeza kuwa na kurasa, barua pepe,namba ya/za simu za kamati , mtu/watu walio maalumu kwaajili ya kushughulikia masuala ya unyanyasaji. Hii itasaidia kuwatia moyo watu kuripoti matukio mbalimbali ya unyanyasaji kwa njia iliyo rahisi na ya haraka kwao.Sambamba na hili kuwe na bodi maalumu ya kusuluhisha masuala ya unyanyasaji yatakayoibuliwa na wanajamii kwa muda ulio mwafaka.
Mwongozo wa UCoC ulenge kuwaunganisha pamoja wahariri wa kujitolea wa miradi ya Wikimedia kote duniani na usiwe na vikwazo vingi sana kiasi cha Wanawikimedia wataona ugumu katika kuchangia katika miradi ya Wikimedia. Pia mwongozo huo ili kuwezesha watu wengi kuwa wanashiriki katika utengenezaji wa sera na kushirikishwa katika maamuzi, kuwe na namna ufiatiliaji wa wanajumuiya kwakuwa mara nyingi watu huweza kuwa na maswali au ushauri mbalimbali kuhusu shirika la Wikimedia Foundation lakini kwa namna moja au nyingine hawawezi kuandika maoni yao hadharani.
Pendekezo lingine lilitolewa kuwa shirika la Wikimedia Foundation lipanue wigo wake wa kusaidia miradi mbalimbali sio tu kujikita katika uhariri wa miradi yake tu. Ilielezwa kuwa shirika linaweza kusaidia miradi mingine mbalimbali inayowaleta wanawikipedia pamoja kama vile michezo na mashindano ya ugunduzi wa kiteknolojia kuhusu nyenzo mbalimbali za kiteknolojia zinazoweza kusaidia kuwaleta pamoja wahariri wa miradi ya Wikimedia.
Ilisahuriwa pia kuwa Shirika la WMF litafute namna ya katika kuwatambua, kuwavutia na kuwapongeza wachangiaji hai katika miradi ya Wikimedia. Kwa mujibu wa wadau ni kwamba kwa sasa kuna upungufu wa njia mahususi za kuwatambua wachangiaji hai wa miradi ya Wikimedia hali inayochangia baadhi ya wachangiaji hai kujisikia michango yao muhimu haitambuliwi na mtu yeyote hasa kutoka shirika lenyewe.
Pia ilipendekezwa kuwa WMF ijaribu kuandaa mfano halisi wa huo mwongozo wa UCoC ili wanajumuiya wapate kuona mwonekano wake katika hali y auhalisia, ilielezwa kuwa hiyo itasaidia watu kutoa maoni na mrejesho zaidi kutokana na mwongozo halisia watakaouona.
Mwisho baadhi ya wachangiaji kutoka jumuiya ya Afrika mashariki walipendekeza kuwa kutokana na baadhi ya jumuiya kukumbana na ugumu wa kufanya miradi ya Wikimedia nchini mwao, Shirika lisaidie jumuiya hizi kuhalalishwa kwa kuwa na nyaraka muhimu zinazoweza kusaidia usajili wa jumuiya hizo hasa kwa zile serikali ambazo zina mtazamo hasi kwa kuhusisha miradi ya WMF na masuala ya kisiasa nchini mwao.
Hadithi Muhimu
Mojawapo ya maoni ya baadhi ya washiriki wa utoaji wa maoni kuhusu UCoC walisema njia ya kuwasiliana na mtu mmoja mmoja ilikuwa ni moja ya njia nzuri ya kuwafikia watu na kupata maoni yao kutoka kwa watu wa aina mbalimbali hususani wanawake ambao maranyingi katika jamii nyingi wameonekana kuachwa nyuma katika masuala ya maamuzi na utoaji wa maoni kuhusiana na mambo mbalimbali katika jamii. Pia ilielezwa kuwa mara nyingi wanawake hasa wale wageni wamekuwa wakirudi nyuma katika masuala ya uongozi na ufanyaji wa maamuzi kwakuwa wanaogopa kuwa labda hawana ujuzi wa kutosha kiasi cha kuchukua majukumui hayo. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya watu walipendekeza kuwe na timu fulani kwa kila jumuiya itakayofanya kazi ya kumfikia kila mwanajumuiya ili kujifunza changamoto zinazowakumba na mitazamp waliyonayo kuhusu uchangiaji katika miradi ya WMF. Kwa mujibu wa washiriki, hiyo itasaidia kubadili kama kuna mitazamo hasi iliyojengeka vichwani mwa watu kuwa labda wanatakiwa kuwa wataalamu bingwa katika kila mada ya miradi ya WMF ndipo wachangie au wachukue majukumu fulani katika juhudi za kuendeleza harakati za WMF.
Vilevile wakati wa ukusanyaji wa maoni ya UCoC mmoja wa wahariri wazoefu wa Wikipedia ya kiswahili na Kiingereza alisema safari ya uchangiaji katika Wikipedia ya Kiingereza haijawahi kuwa rahisi na hata sasa sio rahisi kwakuwa kuna sheria kali na kwa mujibu wa mhariri huyo ni kama kuna aina fulani ya ubaguzi kwa maudhui ya Kiafrika. Mchangiaji huyo wa Wikipedia alisema kuwa mara nyingi amekuwa akibishana na wakabidhi wa Wikipedia ya Kiingereza ambao yeye anaamini hawana uhakika wa kitu gani ni maarufu Afrika kwa muktadha wa mada husika na marejeo yanayothibitisha umaarufu wa nada hizo. Pia aliongeza kuwa katika safari zake za uchangiaji wakati mmoja alichangia kuhusu mwanamuziki mmoja maarufu hapa Tanzania ambaye kwa mujibu wa mchangiaji huyu alikuwa na marejeo ya kutosha na ya kuaminika kuhusu umaarufu wake lakini bado mmoja wa wakabidhi wa Wikipedia ya kiingereza alikataa na kusema hakuona sababu ya mwanamuziki huyo kuwa na vigezo vya kuandikwa katika Wikipedia. Hali hiyo ilimfanya afikiri kuwa labda Wikipedia ipo kwaajili ya watu fulani fulani tu kwa kuwa umaarufu na marejeo vinatumika sana kuzuia maudhui mengi ya Kiafrika kuandikwa katika Wikipedia.
Takwimu za zoezi la Ukusanyaji wa Maoni
Mchakato wa ukusanyaji wa maoni kuhusu mwongozo wa UCoC ulijaribu kuhusisha watu wengi kwa kadri ilivyowezekana ili kutoa nafasi kwa watu kutoa maoni yao kutokana na maeneo wanayotokea na aina ya shughuli wafanyazo ikihusianishwa na uchangiaji katika miradi ya Wikimedia Foundation. Katika mchakato huo takribani watu 304 walifikiwa kwa njia tofauti tofauti. Miongoni mwa njia zilizotumika kupata maoni ya watu kuhusu mwongozo wa UCoC ni pamoja na mjadala katika Wikipedia ya Kiswahili (watu 7 walishiriki), watu 57 walishiriki kwa njia mawasiliano ya WhatsApp, watu 73 walipigiwa simu, watu wa 3 walijibu fomu ya dodoso la google , watu wa 3 walishiriki kutoa maoni wakitokea katika jumuiya wanawikimedia kutoka Afrika mashariki, watu 42 walifikiwa kupitia mitandao ya kijamii huku kukiwa na ushiriki wa watu 22 kupitia kurasa za mitandao hiyo ya kijamii.
Kati ya watu hao walioweza kufikiwa na mwaliko wa kuto maoni, watu takribani 103 waliweza kutoa maoni yao kuhusu mwongozo huo wa UCoC na hivyo ilisaidia kupata picha ya ujumla kuhusu watu wana maoni gani. Kiundani zaidi kuhusu watu walioshiriki katika zoezi hilo, watu wote 103 jinsia zao hazikuweza kutambuliwa hadharani, wageni 7 katika miradi ya Wiki, wakabidhi wa 3 wa Wikipedia ya Kiswahili na watu wa 3 wenye haki mbalimbali za kikabidhi. Matokeo ya jumla kuhusu watu waliotoa maoni yao kuhusu swali la muhimu lililoulizwa kuwa walikuwa na maoni gani juu ya kuanzishwa kwa Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Maadili, watu 64 walisema waliunga mkono wazo hilo, 25 walikuwa na baadhi ya masharti na kutokuunga mkono na watu 14 walionekana kutokukataa wala kukubaliana na wazo.
Zifuaazo ni takwimu zinazoonesha matokeo ya mchakato wa ukusanyaji maoni kutoka kwa wanajumuiya:
Hitimisho
Zoezi la ukusanyaji wa maoni kuhusu Mwongozo wa Kimataifa wa Mwenendo na Maadili kiujumla limesaidia kutoa nafasi kwa jumuiya ya wanawikipedia ya Kiswahili sio tu kutoa mrejesho wa maoni yao kuhusu mwongozo wa UCoC, bali pia kushirikishana uzoefu mbalimbali ambao wanawikimedia wanao wakati wanapotumia na kuchangia katika miradi ya WMF. Kupitia mchakato huu, mawazo mazuri, ushauri, maoni na mapendekezo yaliweza kukusanywa na mengi kati ya hayo yakiwa na lengo la kuzifanya juhudi za harakati za WMF zisonge mbele.
Vilevile zoezi hili la ukusanyaji wa maoni limetoa nafasi kubwa kwa wanajumuiya kushirikishwa katika utengenezaji wa sera na utoaji wa maamuzi juu ya harakati za shirika la WMF. Baadhi ya watu walishauri njia hii ya kuwafikia wanajumuiya na kujua mawazo yao iendelezwe na kwamba inaweza kuwa ni njia nzuri ya kuwafanya watu wengi zaidi kushiriki katika uundaji wa sera na utoaji wa maoni.
Pia kupitia zoezi hilo ziliweza kuonekana njia nzuri za kuwafikia watu katika kukusanya maoni yao kuhusiana ma mada tofauti tofauti ikiwemo zile zihusuzo uundwaji wa sera mbalimbali. Kati ya njia zilizotumika katika ukusanyaji wa maoni, njia ya mawasiliano ya mtu mmoja mmoja ilioneklana kuzaa matunda zaidi kwakuwa ilitoa nafasi kwa watu kuuliza maswali ya papo kwa papo kwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa hayajaeleweka vizuri kwao na baada ya hapo walipata nafasi ya kutoa s maoni yao baada ya kuongezeka kwa uelewa wao.
Kwa upande mwingine zoezi hilo lilisaidia kuelewa changamoto ambazo wanajumuiya hupitia. Moja ya changamoto zilizoibuliwa ni ukosefu wa intaneti kwa baadhi ya watu kitu ambacho kwa kwa namna fulani kinaathiri uwezo wa watu kushiriki katika shughuli za mitandaoni na pia kinaathiri ushiriki wa watu katika mijadala ya mtandaoni katika kurasa za miradi ya WMF. Mbali na kujadili masuala yahusuyo jumuiya, zoezi hilo lilisaidia kutoa nafasi kwa wanajumuiya kutoa mawazo yao na ushauri kuhusu harakati za WMF. Baadhi ya maoni au ushauri ilikuwa ni kwamba kuwe na bidii fulani au kamati itakayojikita kushughulikia masuala ya unyanyasaji na pia wazo la kwamba shirika la WMF liandae nyaraka zitakazo saidia baadhi ya jumuiya zinazokumbana na ugumu katika ufanyaji wa miradi ya Wikimedia Foundation.
Jumuiya ya watu watumiao Kiswahili inatoa shukrani za pekee kwa shirika la WMF kwa kuihusisha katika mchakato huu muhimu wa utengenezaji wa sera na kwamba jumuiya inajisikia kuheshimiwa na kuthaminiwa. Pia shukrani za pekee zinaenda kwa wanajumuiya ya kiswahili wenyewe ikiwemo Watanzania, Waganda, Wanyarwanda, Waburundi na Wakenya na wengine wote kwa utayari wao katika uchangiaji wao wa maoni katika mchakato huo licha ya kwamba mchakato huo umefanyika katika mazingira yenye changamoto ya uwepo wa hali ya ugonjwa wa Corona (COVID-19).